Thursday, April 26, 2012

Panya, Mende Na Wadudu: Lugha Ya Kumalizana



Ni kama watu hupata mdadi wa aina isiyoaminika wakisikia viongozi wao huwaita wenginge kwa majina yajaayo na udharaulifu na uonefu. Kwa viongozi wachache barani Afrika, katika miaka mingi iliyopita kuanzia 1994, hali ya matamshi haya ya ukorofi ilizidi mno. Ukifikiria ni kwa sababu gani viongozi wanaamua kutumia lugha ya kuchochea baadhi ya watumwa wao dhidi ya wengine, unashindwa kupata maana mwafaka. Mara kadhaa, lugha chochezi ilileta maafa wa halaiki kwa njia ya kuwadhalilisha wengine.

Juzi, tulisikia kiongozi wa Sudan, Omar Bashir, akiwaita viongozi wa chama kinachotawala nchini Sudan Kusini (SPLM) wadudu. Bashir alitamka neno hilo akiwa anasherekea hadharani hali ya vikosi vyake kuingia eneo la Panthou/Heglig ambalo lilichukuliwa awali, Aprili 10, 2012 na vikosi vya Sudan Kusini. Maafisa wa Sudan Kusini walisema walisukuma wanajeshi wa Sudan ambao waliwashambulia mbeleni, hadi wakateka kwa nguvu eneo la Panthou. Panthou, ambalo liko chini ya udhibiti wa Sudan, ni eneo lenye mtaji wa mafuta na kisima kikubwa cha mafuta ya kutosha kwa uchumi wa Sudan.

Katika harakati ya kushindwa vitani, mzozo wa maneno ulizidi baina ya pande zote mbili, Sudan na Sudan Kusini. Marekani, Umoja wa Afrika, Umoja wa Mataifa na serikali ya nchi nyingi nyinginzo duniani kote, walilaumu Sudan Kusini kwa kuvuka mpaka hadi Sudan na kupeleka mzozo ugaibuni. Lawama hili lilikuwa zito kibisa kwa serikali ya Sudan Kusini hata wakaondoa vikosi vyao katika eneo la Panthou. Hali hilo iliwaghadhibu wananchi ambao mbeleni walikuwa wanasherekea  ushindi wa wanajeshi wao.

Bashir alichukuwa fursa huo wa umoja wa kimataifa kulilaumu Sudan Kusini, na kuwachochea wenyeji wa nchi yake waone majerani yao kama wadudu. Hali iliyowabidi wananchi wa Sudan kuchoma kwa moto kanisa la wakristu jijini Khartoum. Waafrika wa kiasili wa Sudan Kusini walioko Khartoum waliteseka mikononi mwa raia hadharani katika upuzi lililofuata. 

Mnamo mwaka 1994, tuliona vile mauaji wa halaiki yalisababishwa kwa kuwachochea watu. Nchini Rwnada 1994, mwaka Afrika Kusini ilipata uhuru wake na wananchi walikuwa na furaha tele, na Nelson Mandela akiwa mwangaza mpia wa bara, mambo yalikuwa yanageuka vibaya. Kabila la Hutu lilianza kutekeleza uamuzi wa kuwatimu Watutsi. Wahutu waliwaita wenzao wa Tutsi, mende. Fujo na maiti yaliyotokea katika uhasama huo zilishangaza dunia nzima. Idadi ya watu karibu milioni moja waliuawa.

Katika Majira ya Waarabu, ambapo tulitahamakisha tafiri kubwa ya kisiasa katika Afrika ya Kaskazini, rais wa Libya, Gadafi aliwaita watu wake, ambao walihitaji mabadiliko wa mamlaka wake, kuwa panya. Aliwaonya kwamba atawafukuza katika kila pembe la jiji la Tripoli mpaka awacharaze vyema na vikali. Mwishowe, Gadafi mwenyewe ndiye alikamatwa akijificha ndani ya bomba. Idadi ya watu waliokufa katika harakati za kumwondoa katika mamlaka yake haihisabiki.

Kama ilivyonenwa, haba na haba hujaza kibaba, ni vizuri kufanya lawezakanalo kuzuia hali itakayowaua watu kwa wengi. Maneno yake Bashir ni maneno ya muuaji. Afrika na vilevile dunia nzima inayojali haki za binadamu zikae macho.


No comments:

Post a Comment